Idara ya Kiswahili Imepoteza....
Jumanne, Agosti 19, 2025
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Nairobi inaomboleza kifo cha Profesa John Hamu Habwe, msomi mashuhuri, mwandishi na mlezi wa kizazi cha wasomi wa Kiswahili ambaye alilihudumia Chuo kwa zaidi ya miongo mitatu kwa bidii na uadilifu.
Profesa Habwe alijiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi mwaka wa 1989 kama mhadhiri msaidizi na kupanda ngazi hadi kuteuliwa kuwa Profesa Kamili mwaka wa 2023. Aidha, alihudumu kama Mwenyekiti wa Idara ya Isimu na Lugha (2011–2013) na kisha kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Idara ya Kiswahili (2013–2016).
Alizaliwa tarehe 12 Desemba 1962, na taaluma yake yote ya elimu ya juu—Shahada ya Kwanza, Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu—aliipata katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Katika kipindi cha karibu miaka 40 ya ualimu na utafiti, Profesa Habwe alijulikana kwa kufundisha kwa ari, kuandika vitabu na makala ya kitaaluma, na kuwa kinara katika kushauri na kulea wasomi chipukizi.
Katika rambirambi zake, Profesa Iribe Mwangi, Mwenyekiti wa sasa wa Idara ya Kiswahili, alisema:
“Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu na ulimwengu wa Kiswahili kwa jumla umeathirika pakubwa. Profesa Habwe alikuwa mwalimu bora kwa takribani miaka 37. Alinifundisha kuanzia shahada ya kwanza na baadaye akawa msimamizi wangu wa kwanza wa tasnifu ya Uzamivu. Alinitangulia kama mwenyekiti wa idara hii na nilimshirikisha mara nyingi katika mambo mbalimbali. Aliniongoza kwa hekima katika changamoto nyingi nilizokumbana nazo nikiwa kiongozi mchanga. Nitamkumbuka daima kama mlezi, msomi wa isimu na mwandishi mbunifu.”
Profesa Habwe ameacha hazina kubwa ya kitaaluma ikiwemo vitabu vya isimu, makala za kitaaluma, sura za vitabu, matokeo ya mikutano ya kitaaluma, kazi za kifasihi na kamusi. Ingawa alitambulika zaidi kwa kazi zake za kifasihi, kitaaluma alibobea katika Pragmatiki na Uchanganuzi wa Usemi, ambapo alichapisha maandiko mengi yenye ushawishi mkubwa.
Katika miaka ya hivi karibuni alikuwa akiugua, na Chuo Kikuu kinashukuru kwa mchango wake mkubwa na kinasisitiza kuwa urithi wake wa kielimu utaendelea kuenziwa.
Chuo Kikuu cha Nairobi kinatoa pole kwa familia, jamaa, marafiki, wanafunzi na jumuiya pana ya Kiswahili kwa msiba huu mzito.
Mungu ailaze roho ya Profesa John Hamu Habwe mahali pema peponi.
- Log in to post comments