WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UKUAJI WA KIBIASHARA
OFISI YA KATIBU WA WIZARA
HOJA ZA MAZUNGUMZO ZA BI. BETTY MAINA, CBS, KATIBU WA WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UKUAJI WA KIBIASHARA WAKATI WA MAZUNGUMZO NA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MKATABA WA USHIRIKIANO WA KIBIASHARA BAINA YA KENYA NA UINGEREZA (BAADA YA UINGEREZA KUONDOKA KWENYE UMOJA WA ULAYA)
TAREHE: 14 DESEMBA 2020, SAA MOJA ASUBUHI
MAHALI: HOTELI YA SERENA NAIROBI
- Katibu Mkuu wa Utawala
- Makatibu Wakuu waliopo,
- Wawakilishi wa Vyombo vya Habari mliopo,
- Wageni walioalikwa:
- Mabibi na Mabwana,
Hamjambo!
Utangulizi kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara baina ya Kenya na Uingereza
- Asanteni kwa kuchukua muda mapema asubuhi ya Jumatatu kukutana nasi. Ninafurahi kutangaza kuwa Kenya na Uingereza zilitia saini Mkataba wa Kibiashara siku ya Jumanne tarehe 8 Disemba 2020 katika Ofisi ya Mambo ya nje na Jumuiya ya Madola jijini London.
- Mada kamili ya Mkataba huu ni ''Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Jamhuri ya Kenya, Mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa upande mmoja na Uingereza na Ireland Kaskazini kwa upande mwingine.”
- Mkataba huu wa kihistoria ulitiwa saini na Waziri wa Biashara wa Kimataifa wa Uingereza, Mhe. Ranil Jayawardena, Mbunge, huku nikitia saini kwa niaba ya Jamhuri ya Kenya.
- Wajumbe kutoka Kenya walijumuisha, Balozi Johnson Weru, Katibu Mkuu wa Biashara na Ukuaji wa Kibiashara, ambaye pia ni Mwalikishi Mkuu katika Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi, na Balozi Manoah Esipisu, Balozi wa Kenya nchini Uingereza, pamoja na maafisa wengine waliosaidia.
- Ni takribani wiki moja sasa tangu wakati huo, na kama Wizara, tunahisi kuna haja ya kuzungumza na Wakenya na kuwapa habari kuhusu jinsi tulivyofika hapa, faida watakazopata, na kuangazia hatua zitakazofuata.
- Kufuatia kura ya maoni mwaka wa 2016, Uingereza ilijiondoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU) mnamo tarehe 31 Januari 2020. Kulingana na masharti ya Mkataba wa Kujiondoa, Uingereza itabakia kuwa sehemu ya Umoja wa Forodha ya Umoja wa Ulaya na Jimbo la Forodha la Umoja wa Ulaya hadi tarehe 1 Januari 2021.
- Mkataba wa Kujiondoa uliotiwa saini baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya umeweka Kipindi cha Mpito ambapo nchi zinaweza kuendelea kufanya biashara na Uingereza chini ya taratibu zilizopo za biashara za Umoja wa Ulaya hadi tarehe 31 Disemba 2020. Kipindi hiki kinaipa Kenya nafasi ya kuandaa mbinu za kushiriki katika soko la Uingereza hata baada ya 2020 sheria za Umoja wa Ulaya zitakapofikia mwisho wa matumizi nchini Uingereza. Njia za usalama zinazopatikana ni kupitia kujadili mpangilio wa biashara ya nchi mbili au wa kikanda (Jumuiya ya Afrika Mashariki) au kusubiri Uingereza kuondoa ushuru wa juu unaoruhusiwa chini ya Shirika la Biashara Duniani kwa nchi zinazoendelea kama Kenya.
- Wakitambua uwezekano wa kuvurugika kwa biashara ifikapo mwisho wa Kipindi cha Mpito, Mhe. Uhuru Kenyatta na Mhe. Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza walifanya mazungumzo ya kibinafsi kupitia simu mnamo 4 Julai 2020 na wakakubaliana kuanza mazungumzo ya mpangilio wa biashara ya muda mrefu baada ya Brexit.
Mkondo kuelekea mazungumzo ya Mkataba wa Kiuchumi baina ya Kenya na Uingereza
Kenya ilichukua mtazamo wa njia mbili katika mazungumzo ya mpangilio wa biashara baada ya Brexit, njia zote zilifanikiwa:
- Mtazamo wa Kikanda:
- Mtazamo huu ulikuwa mfumo wa mazungumzo uliopendelewa zaidi kwani mazungumzo yangefanywa kwa kutumia njia sawa na Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya kuhakikisha udumishaji wa uadilifu wa Umoja wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
- Ingawa nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zilikuwa zinakubaliana kwamba hati iliyoridhiwa ya mkataba wa ushirikiano wa kichumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya uwe msingi wa mazungumzo na Uingereza, Mataifa mengine Wanachama walipendekeza kuwa Kipindi cha Mpito kiongezwe hadi tarehe 31 Disemba 2021 ili kutoa nafasi ya mashauriano zaidi kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kibiashara, huku Mataifa mengine Washirika yakiashiria kuwa uchaguzi wao wa kitaifa uliokaribia ulisalia kuwa kipaumbele kwao.
- Ni muhimu kutambua kwamba tofauti na Kenya, ambayo ni nchi ya kepekee isiyo ya maendeleo duni/ nchi inayoendelea katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaainishwa kama nchi za maendeleo duni. Kwa hivyo, kwa mujibu wa hali zao za kimaendeleo nchi zinaweza kuendelea kufanya biashara na Uingereza chini ya mipangilio ya Kila Kitu-Isipikuwa-Silaha (EBA). Kwa kuzingatia hilo, Nchi Washirika wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hazikuwa na maamuzi magumu ya kufanya kulingana na makataa na uvurugaji wa biashara utakaotokea baada ya Brexit.
- Mtazamo wa Nchi mbili:
- Kenya imechukua mikakati muhimu inayotokana na uzoefu unaoatokana mazungumzo ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya. Kama mnavyojua, Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya ulikubaliwa mnamo Septemba 2016 lakini bado haujaanza kutumika kufuatia baadhi ya Mataifa Washirika kutoweza kutia saini na kuridhia Mkataba huo.
- Kufuatia msururu wa mashauriano kati ya Uingereza na Jumuiya ya Afrika Mashariki, Uingereza iliyapa Mataifa Washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki fursa ya kujadili makubaliano ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya kwa misingi ya pande mbili. Kenya, kwa hivyo, ilichukua mtazamo wa njia ya nchi mbili kujadili na kuhitimisha Mkataba.
- Mkataba huu wa sasa unazipa Nchi zingine Washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki njia ya kujiunga/kukubali Mkataba (kukubali) - kupitia utaratibu uliokubaliwa tayari baina ya Kenya na Uingereza katika Mkataba huu.
- Hata pale Kenya ilipochagua mtazamo wa nchi mbili, tuliendelea kuyaeleza mataifa mengine Washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu Mkataba huu. Maelezo ya hivi karibuni yalikuwa tarehe 2 Disemba 2020 wakati wa mkutano wa EAC SCTIFI uliofanyika kuandaa Mkutano wa AUC kwa Wakuu wa Nchi na Serikali wa kujitayarisha kuanza kwa biashara mnamo 1 Januari 2021 chini ya AfCFTA.
- Isitoshe, Kifungu cha 37 cha Utaratibu wa Umoja wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kinaruhusu Nchi Washirika kuhitimisha au kurekebisha makubaliano ya kibiashara na nchi ya kigeni ikiwa masharti ya mpangilio huo hayakinzani na utaratibu huu.
Vidokezo vya Mkataba
- Kenya na Uingereza zilianza mazungumzo mnamo Agosti 2020, Idara ya Taifa ya Biashara na Ukuaji wa Kibiashara ikiratibu na kuongoza mazungumzo kwa upande wa Kenya. Mazungumzo ya kibiashara yalifanywa kupitia mtandao kati ya tarehe 25 Agosti na 23 Novemba 2020.
- Ukweli kwamba tulihitimisha mazungumzo haya kupitia mtandao ni ushuhuda kwamba teknolojia ya mawasiliano na uvumbuzi mwingine wa kiteknolojia unaendelea kuwa sehemu muhimu katika nyanja zote za maisha yetu yakijumuisha sera ya biashara, na maendeleo ya kiuchumi. Janga la COVID-19 kwa kweli limebadilisha jinsi mwingiliano wa ulimwengu, pamoja na mazungumzo ya kibiashara yatakavyokuwa baada ya 2020.
- Kwa hivyo, nimefurahi na kuhisi taadhima kutangaza kwamba Kenya na Uingereza zimehitimisha Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi uliokubaliwa na kuhitimishwa kupitia mtandao.
- Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi uliotiwa saini tarehe 8 Disemba 2020 unarudia vifungu vingi vya Mkatabwa wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya ambavyo vinawezesha ufikiaji wa bidhaa Bila Ushuru - Bila Vipimo kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuenda soko la Ulaya. Mkataba huu ukitekelezwa kikamilifu, utaleta faida kubwa kwa Kenya na washirika wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
- Majadiliano, kuhitimisha, na kutiwa saini kwa Mkataba huu kunaandamana na sera pana ya Serikali ya mageuzi ya uchumi kupanua uwezo wa Kenya wa kuuza nje, kuongeza nafasi za ajira na utajiri kwa raia na kukuza ustawi wa pamoja kulingana na Ruwaza ya Kenya 2030.
- Wizara ya Viwanda, Biashara na Ukuaji wa Kibiashara kwa hivyo imejitolea kujadili makubaliano ya kibiashara ya kikanda na baina ya nchi mbili na washirika muhimu wa kibiashara ili kutimiza lengo hili huku ikiunda mifano ya uwasilishaji kutekeleza mipango kama hiyo.
- Kuna mwongozo wa jumla wa sera, "Mkakati Jumuishi wa Maendeleo na Uendelezaji wa Kitaifa na Uagizaji," unaotoa uelekezi kuhusu utekelezaji wa malengo yaliyotajwa hapo juu. Mkakati Jumuishi wa Maendeleo na Uendelezaji wa Kitaifa na Uagizaji pia unawezesha uafikiaji wa faida kamili kwa wazalishaji (wakulima na watengenezaji), waagizaji na washiriki wengine ambao njia zao za kutafuta riziki zinategemea uongezaji wa thamani kwa bidhaa za kuuza nje.
- Kwa hivyo, Mkataba wa ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Kenya na Uingereza uliotiwa saini utaimarisha umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuhakikisha kuwa bidhaa kutoka Kenya na kanda ya Afrika Mashariki zinaendelea kufika Uingereza bila ushuru - bila vipimo baada ya Brexit. Tumeweka kanuni za asili za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuwezesha wazalishaji wetu kupata malighafi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, kuzichakata Kenya, na kuziuza bila ushuru na bila vikwazo nchini Uingereza.
- Swali moja muhimu ambalo ninataka kujibu ni ikiwa tumefungua milango ya bidhaa za bei rahisi na zilizowekewa ruzuku kutoka Uingereza kuingia kwenye soko letu. Tumezingatia haya kwa kuwa na orodha ya bidhaa muhimu kwa pande zote mbili, ambazo kwa upande wa Kenya zinajumuisha orodha sawa na ilivyo katika Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
- Wakati wa mazungumzo ya makubaliano haya, Kenya na Uingereza zilionesha dhamira thabiti ya kujadili makubaliano ya kibiashara na kiuchumi ambayo yanaheshimu uaminifu wa mkataba na Utaratibu wa Umoja wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kutoa fursa ya kujiunga kwa Nchi Washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hili ni muhimu katika kukuza maendeleo endelevu ya kanda ya Afrika Mashariki na kuhakikisha mapendeleo kwa nchi zenye maendeleo duni.
- Ebu nichukue fursa hii kushukuru kazi ya Washiriki wetu Wakuu kwa kuhitimisha mazungumzo ndani ya ratiba na kudumisha umakinifu wao kwenye lengo hili. Mpatanishi Mkuu kutoka Kenya ni Balozi Johnson Weru, Katibu Mkuu wa Idara ya Serikali ya Biashara na Ukuaji wa Kibiashara. Nataka pia kuzishukuru pande zote zilizounga mkono mchakato wa mazungumzo, pamoja na washiriki kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Umuhimu wa Soko la Uingereza kwa Kenya
- Awali, Kenya ilifikia Uingereza na, isitoshe, soko la Uingereza bila malipo ya ushuru na bila vikwazo/vipimo kwa misingi ya muda mfupi uliotolewa chini ya Sheria ya Uafikiaji wa Soko la Umoja wa Ulaya (MAR) 1528/2007.
- Uingereza imekuwa katika nafasi ya tano katika mauzo ya nje ya Kenya kwa bidhaa za nje ya Kenya kwa thamani ya wastani ya kila mwaka ya Shilingi Bilioni 39 (dola milioni 390) kwa miaka mitano (5) iliyopita (2015 - 2019) - na mauzo makubwa yakiwa maua, kahawa, manjani chai, matunda, mboga, na nguo.
- Mkakati wetu ni kufuata kampeni thabiti ya uuzaji kwa lengo la mwaka wa kwanza wa ongezeko la 5% juu ya mauzo ya sasa katika soko la Uingereza. Miaka inayofuata itakua kwa kuongezeka kwa kiwango sawa au faida za juu. Kwa mfano, nitaendelea kwa kuwapa takwimu kadhaa.
- Sehemu ya soko ya mauzo ya nje ya Kenya katika Umoja wa Ulaya ya wastani kwa Ksh. Bilioni 133 kwa mwaka, na mauzo ya nje yanayolenga Uingereza yakiwa tariban 30% ya sehemu ya soko la Umoja wa Ulaya.
- Takwimu za sasa za biashara ya muda mfupi kufikia Agosti 2020 zinaonyesha mauzo ya nje ya Kenya yalikuwa na thamani ya Ksh. Bilioni 34.9 (dola milioni 337.7), huku uagizaji ulikuwa na thamani ya Ksh. Bilioni 18.9 (dola milioni 185.2) katika kiwango cha wastani cha ubadilishanaji wa Ksh. 103 kwa dola 1, na ulinganifu wa biashara wa Ksh. Bilioni 15.9 (dola milioni 154.5), kwa upande wa Kenya.
- Katika Sekta ya Kilimo, kahawa, maua, na manjani chai zilisalia kuwa bidhaa muhimu kwa mauzo ya nje ya Kenya. Uchanganuzi wa soko la Uingereza unaonyesha kuwa:
- Uingereza inaagiza kahawa yenye thamani ya dola bilioni 1 kutoka ulimwengu, huku Kenya ikiuza kahawa yenye thamani ya dola milioni 7.8, ambayo ni asilimia 0.8 tu ya soko hili. Ikiwa sehemu ya Kenya katika soko la Uingereza ingeongezeka kwa 5% ifikapo mwaka 2025, tungepata mauzo ya nje ya ziada ya thamani ya dola milioni 52, ambayo bado iko chini ya uwezo wa mauzo ya kahawa ya Kenya yanayokisiwa kuwa takriban dola bilioni 1.05.
- Uingereza inaingiza manjani chai yenye thamani ya dola bilioni 356 kutoka ulimwenguni kote, huku Kenya ikiuza manjani chai yenye thamani ya dola milioni 150 kwa Uingereza, ambayo ni asilimia 42.4 ya soko hilo.
- Kwa upande wa kunde na Viungo, uwezo wa wakulima wa Kenya wa kuuzia Uingereza bidhaa ni mkubwa na haujazingatiwa. Uingereza inaagiza mazao ya jamii ya kunde (maharagwe, mbaazi, ndengu, n.k.) yenye thamani ya dola milioni 249 kutoka kote ulimwenguni, huku Kenya ikiuzia Uingereza kunde zenye thamani ya dola milioni 32. Ikiwa sehemu ya Kenya katika soko la Uingereza ingeongezeka kwa 5% ifikapo mwaka 2025, hii ingekuwa mauzo ya nje ya ziada ya thamani ya dola milioni 12, ambayo bado iko chini sana ya uwezo wa mauzo ya mazao ya kunde inayokaridiriwa kuwa takriban dola milioni 240.
- Soko lililojumuishwa la uingizaji wa bidhaa za viungo vinavyoliwa Uingereza, ikiwa ni pamoja na pilipili, tangawizi, zafarani, bizari, mdalasini, majani ya viungo, na viungo vingine, vina thamani ya takriban dola za milioni 234, huku Kenya ikiuza nje asilimia 1.5 pekee ya idadi hiyo ingawa ina uwezo wa kuuza nje viungo vya thamani ya dola milioni 232.
- Uingereza imekuwa soko la jadi la Maua kutoka Kenya, Matunda, na Mboga, lakini bado hatujafikia kiwango kinachofaa. Uingereza inaagiza matunda yenye thamani ya dola bilioni 6.3, huku Kenya ikiiuzia matunda yenye thamani ya dola milioni 5, ambayo ni asilimia 0.1 tu ya soko hili. Kenya inakadiriwa kuwa na uwezo wa mauzo ya nje ya matunda yenye thamani ya dola bilioni 6. Ikiwa Kenya ingepanua mauzo yake ya nje kwa 5%, mauzo hayo yangeongezeka kwa dola milioni 314.
- Kwa upande wa mboga, soko la Uingereza la ununuzi linakadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 4.3, huku Kenya ikipeleka mauzo ya nje ya 2.3% katika soko hilo. Uwezo wa Kenya wa mauzo ya nje ya mboga kwenda Uingereza unakadiriwa kuwa dola bilioni 4.2
- Kenya inauzuia Uingereza maua yenye thamani ya dola milioni 105. Uwezo wetu wa mauzo ya nje wa sekta ya maua kwa Uingereza unakadiriwa kuwa dola bilioni 10.
- Katika sekta ya uzalishaji/utengenezaji bidhaa, kuna msisitizo katika kuchakata bidhaa za kilimo, Nguo na Mavazi, Ngozi na Viatu, Chuma na Bidhaa zake, Kemikali na bidhaa zake, Dawa na vifaa vya Kimatibabu, Plastiki na Mipira, Uhandisi wa Umeme, vifaa vya Magari na Samani.
- Kwa mfano, kwa Nguo na Mavazi, soko la uagizaji la Uingereza lina thamani ya dola bilioni 27.7, huku Kenya ikiuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 2 tu japo ina uwezo wa mauzo ya nje ya nguo na mavazi zenye thamani ya dola bilioni 1 tukifufua viwanda vyetu, jambo ambalo Wizara yangu inashughulikia kwa sasa.
- Mambo ni vivyo hivyo kwa uzaaji wa Ngozi na Viatu, ambapo Kenya inauza bidhaa za thamani ya dola milioni 0.9, ilhali tuna uwezo wa kustawisha viwanda vya ngozi.
- Sekta ya uvuvi na njia za usambazaji zinazohusika zinatoa uwezekano mkubwa na ambao haujachunguzwa wa kuuza kwenye soko la Uingereza lenye thamani ya takriban dola bilioni 3.
- Pamoja na Mkataba huu, pia tumefungua soko la kuuza nje kwa Sekta ya Mifugo, tukilenga Wanyama walio hai, Nyama, Maziwa, na Asali. Kwa mfano, soko la uagizaji wa asali la Uingereza lina thamani ya takriban dola milioni 111. Kenya kwa sasa haiuzii Uingereza asali yoyote, lakini ina uwezo wa kuuza asali ya kutosha kwa soko la Uingereza.
- Uingereza pia ni miongoni mwa nchi Kenya inapoagiza bidhaa nyingi, hususani vifaa vya uzalishaji (mashine), magari, dawa, vitabu vilivyochapishwa na bidhaa zingine za karatasi, na vifaa vya umeme na kielektroniki. Mwaka wa 2019, uagizaji wa Kenya kutoka Umoja wa Ulaya ulijumuisha Shilingi Bilioni 235, huku uagizaji kutoka Uingereza ukikadiriwa kuwa 14.9% (takribani Shilingi bilioni 35) ya hela hizi.
- Kwa hivyo, Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Kenya na Uingereza tuliotia saini unatarajiwa kuchochea ukuaji na upanuzi wa mauzo ya nje katika sekta zingine za kipaumbele na njia za uongezaji wa thamani zilizoainishwa katika Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Maendeleo na Uendelezaji wa Uagizaji wa nje, ikijumuisha kilimo, utengenezaji, uvuvi, mifugo na mapambo ya nyumba ambapo Kenya ina uwezo mkubwa wa kuuza nje.
- Katika mazungumzo ya siku zijazo kuhusu biashara, Kenya itafuatilia mazungumzo ya uwekezaji, huduma, biashara ya kidijitali, ambayo ni muhumu katika kuimarisha uvumbuzi wa njia za kuongeza thamani. Umuhimu wa haya umezidishwa na janga la COVID 19 linaloshuhudiwa kote ulimwenguni.
Hatua zinazofuata Kuelekea Uridhiaji na Utekelezaji
- Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi uliotiwa saini lazima upitie michakato ya ndani inayofaa, pamoja na kuridhiwa na Bunge, kabla ya kuanza kutumika kufikia 1 Januari 2021. Wizara imeanza mazungumzo na uongozi wa Bunge la Kitaifa kuhusu suala hili.
- Baadaye, kutakuwa na maandalizi na utekelezaji wa sheria ya uridhiaji na Wizara ya Mambo ya nje.
- Wakati wa mazungumzo ya Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Kenya na Uingereza, suala lilokuwa linajirudia mara kwa mara ni kuhusu ushirikishwaji wa wadau, na ushiriki mkubwa wa washirika wasio wa kiserikali, ikiwa ni pamoja na mashirika katika sekta binafsi. Kama Wizara, tunapanga kuendelea na shughuli hizi tunapoelekea kwenye utekelezaji.
- Mashirika ya vyombo vya habari ni wadau wetu wakuu, na ndiyo sababu ya mkutano huu. Ninawakaribisha kuendelea kushirikiana nasi ili tuweze kuhamasisha wananchi kote nchini kuhusu fursa ambazo Serikali imeunda kupitia Mkataba huu na kazi zingine tunazofanya katika Wizara.
Asanteni na Mkae Salama!
Nawa mikono kila mara na uvae barakoa!
- Log in to post comments