MWITO WA IKISIRI Kongamano la Chaukidu la Mtandaoni 2021 Mei 21-22, 2021

MADA KUU: Hali ya Ufundishaji Kiswahili Ulimwenguni Sasa na Baadaye

Kiswahili ni miongoni mwa lugha za Kiafrika na za Kimataifa inayozungumzwa na watu takriban milioni 150 ndani na nje ya bara la Afrika. Pia, ni lugha inayotumika katika kutekeleza majukumu anuwai yakiwemo elimu, siasa, biashara n.k. Katika mkabala huo, Kiswahili kinaibuka kama Lingua Franka Afrika Mashariki na mataifa kadha barani Afrika. Mbali na kuwa lugha muhimu Afrika, Kiswahili kinatumika pia kote ulimwenguni kwa namna moja au nyingine, kwa mfano katika ufundishaji, uanahabari, utafiti, uanaharakati, n.k. Kwa mantiki hiyo, na kutokana na matukio ya sasa duniani, Chama cha Ukuzaji wa Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kimeandaa kongamano litakalozungumzia hali ya ufundishaji wa Kiswahili ulimwenguni kwa sasa, hasa kipindi hiki cha Korona, na athari zake katika siku za usoni. Kongamano hili ambalo litafanyika mtandaoni, litawaleta pamoja wataalamu wa Kiswahili kutoka Afrika pamoja na mataifa mengine ulimwenguni kubadilishana mawazo. Kongamano litafanyika Mei 21-22, 2021. Tafiti/makala zinaweza kuangazia nyanja anuai kama vile:

1. Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili katika Kipindi cha Janga la Korona.

2. Kiswahili na Maendeleo Endelevu katika Jamii.

3. Kiswahili na Teknolojia

4. Kiswahili na Mazingira ya Ufundishaji/Ujifunzaji

5. Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kiswahili kama Lugha ya Pili/Kigeni

6. Ubunifu na Ugunduzi katika Ufundishaji wa Kiswahili wakati wa Korona

7. Kiswahili, Elimu na Afya.

8. Uundaji, Usambazaji na Usawazishaji wa Istilahi za Kiswahili.

9. Pedagojia katika Taaluma za Lugha, Isimu na Fasihi

10. Utafiti, Uandishi na Uchapishaji wa Vitabu vya Kiswahili 

 

Ikisiri zote zitumwe kupitia fomu maalumu ambayo inapatikana katika kiungo hiki: https://chaukidu.org/ikisirikongandao2021/ Kwa swali lolote kuhusu kongamano la Mtandaoni 2021, wasiliana na Kamati-Andalizi, kwa barua-pepe kwenda kongandao@gmail.com. Hakuna ikisiri itakayopokelewa kwa barua-pepe. Tuma kwa kutumia kiungo ulichopewa hapo juu. Kwa taarifa Zaidi kuhusu kongamano hili, tembelea tovuti ya CHAUKIDU: http://chaukidu.org/kongandao2021