Webina liyoandaliwa na Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi Kusherehekea Miaka 50 ya Jubilee

Webina liyoandaliwa na Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi Kusherehekea Miaka 50 ya Jubilee

Siku Jumatano tarehe 2, Disemba, 2020, Idara ya Kiswahili kupitia kamati andalizi, iliandaa webina  kusherehekea miaka 50 tangu Chuo Kikuu cha Nairobi kilipoanzishwa rasmi. Kauli Mbiu ya webina ilikuwa, “Kiswahili Ulimwenguni.”

Webina hiyo ya kufana ilihudhuriwa na watu wengi ajabu wenye tajriba mbali wakiwemo wataalamu na wasomi kutoka sehemu mbali za ulimwengu kama vile Poland, Ghana, Uganda, Tanzania, Marekani na Uchina (wakiongozwa na  Prof. Ngugi wa Thiong’o), wahadhiri na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Pamoja na vyuo vingi vingine.

Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Prof. Stephen Kiama ambaye alifungua webina hiyo kirasmi alinena kuwa Chuo Kikuu cha Nairobi kinajivunia kwa kuweza kuchangia pakubwa usambazaji wa lugha ya Kiswahili duniani. “Chuo Kikuu cha Nairobi kimeorodheshwa miongoni mwa vyuo vikuu 10 bora barani Afrika mara kwa mara na tuna furaha kwamba mchango wetu kwa jamii na umma ni wa kiwango kikubwa zaidi.” Prof Kiama aliongeza kwamba Chuo Kikuu Cha Nairobi kitaendelea kuweka mikakati bora ili kufanikisha uchapishaji, utafiti na uvumbuzi wa lugha ya Kiswahili. “Nina furaha kuwajulisha kwamba wahadhiri na maprofesa wa Idara hii ya Kiswahili wametia fora katika ufundishaji, utafiti na uchapishaji. Ni vigogo wanaotajika ulimwenguni kote na baadhi wameweza kushinda tuzo za kitaifa na za kimataifa”.

Naibu Makamu wa Chuo Kikuu cha Nairobi anayesimamia maswala ya Elimu Prof. Julius Ogeng’o katika hotuba yake aliwapongeza walimu na wataalamu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Naiobi kwa kupeperusha  bendera ya Chuo kikuu ulimwenguni kupitia ufundishaji, utafiti na uchapishaji kwa lugha ya Kiswahili. “Kama tunavyofahamu sote, Kiswahili ni lugha rasmi na lugha ya taifa la Kenya. Kwa hivyo,tunajivunia ukweli kwamba lugha hii inazidi  kusambaa ulimwenguni”, alisema Prof. Ogeng’o.

 

Kwa upande wake, msomi mtajika Prof. Ngugi wa Thiongo ambaye ndiye alitoa hotuba maalum katika webina hiyo alisema kwamba ni muhimu kuwepo na sera ambayo inazipa kipao mbele lugha tatu nchini Kenya zikiwemo, lugha ya mama, Kiswahili na Kiingereza. Akimnukuu Shabaan Robert, Prof. Ngugi wa Thiongo alisema kwamba, Titi la mama litamu, hata likiwa la mbwa, Kiswahili naazimu, sifayo iliyofumbwa, Kwa wasiofahamu, niimbe ilivyo kubwa, toka kwa milizamu, funika palipozibwa, titile mama litammu, jingine halishi hamu.

Dkt. Beata Wojtowicz kutoka nchi ya Poland alisema kwamba Kiswahili kinaenziwa sana nchini humo na kwamba lugha  za Afrika haswa Kiswahili ni muhumu sana katika mawasiliano duniani.

Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili, Prof. Iribe Mwangi naye alisema kwamba kaulimbiu ya webina hiyo ilikuwa na madhumuni  kuzungumzia namna ambavyo Chuo Kikuu cha Nairobi kimechangia katika kukisambaza na kukizagaza Kiswahili ulimwenguni. Prof. Iribe alisema kwamba “ni muhimu kutaja kwamba kati ya masomo yote tunayoyatoa humu chuoni, ni Kiswahili pekee chenye asili yake humu, masomo mengine yote tumeyakopa. Hivyo basi, kama waghaibuni wametufanyia hisani na kutuletea uhandisi, uhasibu, sheria, utabibu, fizikia, falsafa na maarifa mengineyo, mbona sisi tuwahini kile tunachokimiliki?” Prof.  Iribe vile alitoa mifano kuonyesha namna ambavyo Kiswahili kilienezwa ulimwenguni katika miaka 50 iliyopita. “Katika miaka ya 70, wasomi kama vile Prof. Mohamed Abdulaziz walieneza Kiswahili Ulaya, hasa Ujerumani na Uingereza. Baadaye, wasomi wengine kutoka chuoni humu kama Maprofesa Wamitila, Rayya Timammy na Kineene walifuata nyayo hizo. Prof. Said Ahmed na Prof. Kineene walieneza Kiswahili Ujapani naye Dkt. Hannah Mwaliwa akakiendeleza Afrika Kusini. Dkt. Ayub Mukhwana na baadaye Prof. Olali walifunza Kiswahili Uchina. Katika miaka ya themanini, Prof. Kineene alifunza Kiswahili Korea Kusini katika Chuo Kikuu cha Hankuk. Baadaye, walimu wengi wamesaidia kukuza kitengo cha Kiswahili chuoni humo wakiwemo Maprofesa Tom Olali na Kithaka wa Mberia na pia Dkt. Nyachae Michira. Maprofesa Lisanza Muaka na Iribe Mwangi wamesambaza Kiswahili Marekani Kusini na Marekani Kaskazini. Dkt. Prisca Jerono naye aliwahi kukipeleka Kiswahili Marekani ya Kati na Afrika Magharibi. Maprofesa Mohamed Bakari, Iribe na Mbuthia wote wamewahi kukieneza Kiswahili Uarabuni kwa njia moja au nyingine. Mwisho, Maprofesa Mbatiah na Mberia na pia Madaktari Michira, Mungania na Zaja wote wamewahi kufunza Kiswahili Marekani. Hawa ni baadhi tu ya walimu wa Kiswahili ambao wamekitoa Kiswahili Chuoni (nchini) na kukisambaza ulimwenguni.” Kwa niaba ya Idara, Profesa Iribe aliuomba usimamizi wa Chuo Kikuu cha Nairobi ufikirie kubadilishaji sera ya lugha Chuoni ili lugha ya Kiswahili iweze kutumika katika sherehe za mahafali. Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi Prof. Kiama alijibu kwamba ombi hilo linaweza kutekelezwa japo kwa hatua.  

Webina hiyo ya Idara ya Kiswahil iliandikisha rekodi kwa kuhudhuriwa na zaidi ya watu 500.