Somo la Kiswahili limegawa katika vitengo vitatu:
- Fasihi
Sanaa au tawi la sanaa linatumia lugha katika kufikisha ujumbe wa msanii kwa hadhira.
- Isimu/ Lugha
Tawi la isimu (au "maarifa ya lugha) linahusu uchunguzi wa lugha kisayansi. Limegawa katika matawi mbalimbali:
- fonetiki – Inahusu sauti zinazotolewa na binadamu
- fonolojia- Tawi hili linahusu mfumo wa sauti katika lugha maalum
- mofolojia- Hushughulikia mfumo wa maneno
- sintaksia- hushughulikia sentensi
- semantiki- hushughulikia maana
- Pragmatiki- hushughulikia matumizi ya lugha katika muktadha mahususi
- Isimujamii- Hushughulikia uhusiano kati ya lugha na jamii
3. Tamrini (Skills)
Kitengo hiki kinahuzisha mbinu za mawasiliano kama vile kusikiliza, kuzungumza kusoma na kuandika.
Faida za Kusoma Kiswahili
- Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Kenya na kwa kiasi kikubwa inaeleweka na kutumiwa na Wakenya wengi kwa ajili ya mawasiliano ya kila siku. Katiba mpya inakitambua Kiswahili kama lugha rasmi sambamba na Kiingereza. Ni wazi kuwa hali hii mpya itachangia pakubwa katika kutimizwa kwa ndoto ya wasomi wa Kiswahili na hata viongozi wa kisiasa barani Afrika ambao wamekuwa wakipendekeza kuwa Kiswahili kiwe lugha inayotumiwa katika shughuli rasmi kote barani Afrika.
- Kwa sasa Kiswahili ndiyo lugha rasmi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na imependekezwa kama lugha mojawapo ya Muungano wa Afrika. Isitoshe, Kiswahili ni lingua franca katika eneo zima la Afrika Mashariki na hata Kati. Hivyo, kuifahamu lugha hii kwa ufasaha utaleta manufaa si haba ikiwemo ajira.
- Kuwezesha uandishi wa vitabu, majarida, habari, utangazaji, magazeti, blogu na mengine mengi ya kuleta mapato.
- Huwezesha ufundishaji, ndani nan je ya nchi katika vitengo mbalimbali
- Tafsiri na ukarimani katika kitengo cha kimataifa ni matunda ya kujifunza Kiswahili kikamilifu
- Kiswahili hutumiwa katika mikutano ya siasa na ni lugha ya Bunge, hivyo kuna umuhimu wa kuijua
- Biashara kati ya nchi moja na nyingine huendeshwa kwa lugha inayoeleweka kwa pande mbili zinazohusika hasa katika Afrika Mashariki. Ni wazi kuwa biashara ni muhimu katika uimarikaji wa uchumi wa nchi yoyote. Hivyo basi, matumizi ya Kiswahili katika biashara ya kimataifa, yanatarajiwa kupewa kipaumbele kama njia ya kukuza lugha ya Kiswahili. Hali hii inaweza kuendeleza biashara, hususani kati ya nchi ambazo hutumia Kiswahili kwa mawasiliano.
- Lugha ya Kiswahili ndiyo inayotumika katika mawasiliano mabana katika jamii. Hivyo, masilahi ya jamii kama vile kilimo, malezi n.k hushughulikiwa na kufikiwa vyema kupitia matumizi ya lugha ya Kiswahili.
- Sayansi na teknolojia huenezwa kwa lugha rasmi. Maendeleo katika uwanja huu ni muhimu kwa nchi yoyote ulimwenguni. Maarifa katika sekta hiyo ni kichocheo kikuu cha ustawi wa jamii, hususani kiuchumi. Ili lugha ya Kiswahili iweze kutumika katika shughuli za kisayansi na kiteknolojia, istilahi za kurejelea masuala mbalimbali husika zitahitaji kubuniwa na kusanifishwa. Ni kupitia juhudi hizi ambapo lugha hii itakuwa na uwezo wa kutumika katika sekta hii huku ikikumbukwa kuwa dhana husika ni ngeni na zimekuwa zikirejelewa kwa Kiingereza kwa miaka mingi. Teknolojia ya mawasiliano na tovuti, hutumia lugha ya Kiingereza kwa kiasi kikubwa. Hapa ndipo lugha ya Kiswahili itahitaji kuimarishwa ili ichukue nafasi muhimu katika mawasiliano ya aina hiyo.
- Kutokana na hadhi mpya, Kiswahili kinatarajiwa kuanza kutumiwa kufundishia masomo mengine katika viwango mbalimbali vya elimu nchini. Maandalizi yatahusu utayarishaji wa mitalaa mipya ya elimu katika viwango mbalimbali. Aidha, vitabu vitakavyohitajika ili kufundishia masomo katika viwango anuwai vya elimu sharti viandikwe kwa Kiswahili. Mafunzo kwa walimu vyuoni yanatarajiwa kufanywa kwa Kiswahili kama njia ya kuwaandaa wahusika kufundisha katika taasisi za elimu nchini. Maafisa wa elimu katika ngazi tofautitofauti watahitajika kujifunza Kiswahili ili kujitayarisha kwa jukumu la kuelekeza mipango ya elimu katika maeneo yao. Hali hii inatarajiwa kudhihirika katika taasisi za elimu ya juu kama vile vyuo vikuu ambavyo vitatakiwa kuweka mikakati imara ya kuziwezesha kuimarisha mawasiliano kwa Kiswahili miongoni mwa wataalamu wa masomo mbalimbali. Hii inamaanisha kuwa lugha ya Kiswahili imestawishwa sambamba na Kiingereza kuitayarisha kukidhi mahitaji ya kufundishia masomo mbalimbali.
- Dini nyingi hutumia Kiswahili ili kuwafikia hadhira kubwa. Wengine hutumia wakalimani katika mahubiri yao.
Sababu hizi na zingine nyingi, ni ishara tosha kwamba Kiswahili ni lugha ya dhahabu’ ambayo tunaionea fahari.
Idara ya Kiswahili inatoa mafunzo ya aina nyingi yanayonuia kukidhi mahitaji ya jamii ya kisasa kwa kuwafunza wanafunzi wetu maarifa na ujuzi wa aina tofauti. Mafunzo hayo hutolewa kupitia kwa kozi mbalimbali zinazo mtayarisha mwanafunzi kikamilifu. Kwa habari zaidi kuhusu kozi hizo tembelea tovuti ya idara: https://kiswahili.uonbi.ac.ke/admission-view)
Aidha, idara ya Kiswahili ina waalimu ambao ni waandishi mashuhuri wa kutajika ulimwengu kote chini ya uongozi wa mwenyeketi wa idara Prof. Iribe. (habari zaidi kuhusu waalimu tembelea tovuti ya idara: https://kiswahili.uonbi.ac.ke/staff)