Wahadhiri wetu Watafsiri Kanuni za Bunge la Kitaifa

Waadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi ni miongoni mwa wanajopo walioshiriki katika kutafsiri Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa kwa Kiswahili zilizozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta mnamo tarehe November 12, 2020.

 

Kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Iribe Mwangi ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili alikuwa kiongozi wa jopo la wataalamu wa Kiswahili  ilhali Dkt. Prisca Jerono na Dkt. Nyachae Michira wakiwa wanachama wa kikosi hicho.

 

"Hii ni hatua ya pili kubwa kuhusu utumiaji wa Kiswahili katika mijadala ya bunge baada ya ya hatua ya awali kufanywa  mnamo 1974 kufuatia agizo kutoka kwa mwanzilishi wa taifa Mzee Jomo Kenyatta," alisema Mhe. Justin Muturi, Spika wa Bunge la Taifa. "Kutafsiri kanuni za Bunge kwa lugha yoyote si kazi rahisi kwani kanuni zinaambatana na lugha ya kisheria. Hii ni taaluma ya kipekee.  Kazi waliofanya maafisa wetu pamoja na wataalamu ni ya kuridhisha mno kwani walichangia pakubwa kufanikisha kazi hii."

 

Rais Kenyatta alizindua toleo la Kiswahili la maagizo ya Bunge yaliyopewa jina la Kanuni za Kudumu Za Bunge la Taifa baada ya kuhutubia kikao cha pamoja cha Bunge ambapo pia Rais alitoa Hotuba ya Mwaka kulingana na mahitaji ya katiba.

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Nairobi  Profesa Stephen Kiama alikuwa mgeni aliyealikwa katika Bunge wakati wa hafla hiyo. Kabla ya sherehe ya uzinduzi, Mkuu wa Chuo na wataalamu hao walipokea utambulisho wa kipekee na Spika wa Bunge  katika kikao cha pamoja cha Bunge.

Hongereni Wahadhiri kwa kazi nzuri mlioifanya.