Hotuba ya Mwenyekiti wa Idara ya kiswahili Chuo Kikuu cha Nairobi kwenye Webina kusherehekea miaka hamsini tangu kuasisiwa kwa Chuo Kikuu cha Nairobi mnamo tarehe 2 Desemba, 2020

Profesa Iribe Mwangi, Mwenyekiti Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Nairobi

 

• AFISA MKUU MTENDAJI WA TUME YA ELIMU YA

VYUO VIKUU, PROF. MWENDA NTARANGWI,

  • MAKAMU WA MKUU WA CHUO KIKUU CHA NAIROBI, PROF. STEPHEN KIAMA,
  • PROFESA MTAJIKA NGUGI WA THIONG’O
  • NAIBU MAKAMU WA MKUU WA CHUO KIKUU CHA NAIROBI, ANAYESIMAMIA MASWALA YA ELIMU PROF. JULIUS OGENG’O
  • MTIVA WA KITIVO CHA SANAA, PROF. EPHRAHIM WAHOME,
  • WAHADHIRI WA IDARA YA KISWAHILI NA WAHADHIRI WENGINE WOTE,
  • VIONGOZI MBALIMBALI WA CHUO KIKUU CHA NAIROBI MLIOPO,
  • WALIMU NA WANAFUNZI,

• WAPENZI NA WAKEREKETWA WA KISWAHILI,

  • WAGENI WAALIKWA,
  • WAHESHIMIWA MABIBI NA MABWANA,
  • NAWAPA SALAMU ZANGU ZA DHATI!

Ni furaha yangu kusema machache kuhusu webina hii. Hata hivyo, kabla ya kufanya hivyo, naomba nitoe shukrani zangu kwa nyote ambao mmeungana nasi siku ya leo tunapozungumza kuhusu maenezi ya Kiswahili ulimwenguni.

Kaulimbiu ya Webina hii ni “Kiswahili Ulimwenguni” na tunanuia kuzungumzia namna ambavyo Chuo Kikuu cha Nairobi kimechangia katika kukisambaza na kukizagaza Kiswahili ulimwenguni. Ni muhimu kutaja kwamba kati ya masomo yote tunayoyatoa humu chuoni, ni Kiswahili pekee chenye asili yake humu, masomo mengine yote tumeyakopa. Hivyo basi, kama waghaibuni wametufanyia hisani na kutuletea uhandisi, uhasibu, sheria, utabibu, fizikia, falsafa na maarifa mengineyo, mbona sisi tuwahini kile tunachokimiliki?

Ni kutokana na uelewa huu ambapo Chuo hiki kimekuwa katika mstari wa mbele kukisambaza Kiswahili ulimwenguni. Naomba nitoe mifano kuonyesha namna ambavyo hili limetekelezwa katika miaka 50 iliyopita.

Katika miaka ya 70, wasomi kama vile Prof.

Mohamed Abdulaziz walieneza Kiswahili Ulaya, hasa Ujerumani na Uingereza. Baadaye, wasomi wengine kutoka chuoni humu kama Maprofesa Wamitila, Rayya Timammy na Kineene walifuata nyayo hizo. Prof. Said Ahmed na Prof. Kineene walieneza Kiswahili Ujapani naye Dkt. Hannah Mwaliwa akakiendeleza Afrika Kusini. Dkt Ayub Mukhwana na baadaye Prof Olali walifunza Kiswahili Uchina. Katika miaka ya themanini, Prof. Kineene alifunza Kiswahili Korea Kusini katika Chuo Kikuu cha Hankuk. Baadaye, walimu wengi wamesaidia kukuza kitengo cha Kiswahili chuoni humo wakiwemo Maprofesa Tom Olali na Kithaka wa Mbera na pia Dkt. Michira. Maprofesa Lisanza Muaka na Iribe Mwangi wamesambaza Kiswahili Marekani Kusini na Marekani Kaskazini. Dkt. Prisca Jerono naye aliwahi kukipeleka Kiswahili Marekani ya Kati na Afrika Magharibi. Maprofesa Mohamed Bakari, Iribe na Mbuthia wote wamewahi kukieneza Kiswahili Uarabuni kwa njia moja au nyingine. Mwisho, Maprofesa Mbatiah na Mberia na pia Madaktari Michira, Mungania na Zaja wote wamewahi kufunza Kiswahili Marekani.

Hawa ni baadhi tu ya walimu wa Kiswahili ambao wamekitoa Kiswahili Chuoni (nchini) na kukisambaza ulimwenguni. Usambazaji huu hutokana na mapenzi wahadhiri hawa waliyonayo kwa Kiswahili. Kiswahili hukuza sio tu jina la Chuo Kikuu cha Nairobi bali pia jina la nchi yetu. Kwetu, kueneza Kiswahili ni kitendo cha uzalendo. Sote twajua kwamba katika mataifa ya nje, Kiswahili hunasibishwa na mataifa mawili pekee: Kenya na Tanzania. Ni fahari kubwa sana kwetu Kiswahili kinaposambaa ulimwenguni na ni azima yangu kuwa hili litaendelea.

Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Nairobi, sasa naomba kwa unyenyekevu niseme nawe. Nilibahatika kuandamana nawe hadi Bungeni wakati Kanuni za Kudumu za Bunge la Taifa zilipozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta. Kwa hivyo sasa Kiswahili kinatumika Bungeni. Vilevile Kiswahili ni lugha rasmi kikatiba. Ombi la Idara ni kwamba Chuo Kikuu cha Nairobi, kama ilivyo kawaida yake kuongoza, kiwe Chuo Kikuu cha kwanza nchini (labda hata ulimwenguni) kufanya mahafali (graduation ceremony) yake kwa Kiswahili. Tutafurahia sana hili likifanyika na kama Idara tutakuwa radhi kusaidia. Kwa niaba ya Idara, nawakaribisha kwenye webina hii kwa moyo mkunjufu.