KUBIDHAISHA KISWAHILI:

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu Makubaliano ya Kibiashara baina ya Kenya na Uingereza - 

 

Je, Kiswahili kinaweza kunufaisha vipi kufuatia mchakato huu wa biashara?

 

 

 

                                           JAMHURI YA KENYA

               WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UKUAJI WA KIBIASHARA

          IDARA YA SERIKALI YA BIASHARA NA UKUAJI WA KIBIASHARA

______________________________________________________

 

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara kuhusu Makubaliano ya Kibiashara baina ya Kenya na Uingereza

 

Je, muktadha wa mazungumzo ya makubaliano kuhusu Biashara na Uchumi baina ya Kenya na Uingereza ni upi?

Kenya na Uingereza zimehitimisha na kutia saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) ambao umeundwa kulinda maslahi ya nchi hizi mbili, na eneo pana la Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kijiondoa kwa Uingereza kutoka kwa Jumuiya ya Ulaya (Brexit). Ushirikiano huu wa kibiashara umekuwa ukipitishwa kwenye michakato ya uridhiaji na Mabunge ya Kenya na Uingereza.

Makubaliano haya yanafafanua athari za Ushirikiano wa Kibiashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa Umoja wa Ulaya. Makubalinao haya yatasaidia bidhaa kutoka Kenya na nchi washirika wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kufikia masoko ya Uingereza na Ulaya, bila ushuru au vizuizi.

Ushirikiano huu wa Kibiashara umewekewa msingi na Ushirikiano wa Kimkakati uliokubaliwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson. Unajumuisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoa jukwaa bora kwa Uingereza, Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki nzima, kupanua ushirikiano wao wa kibiashara na kiuchumi na Uingereza.

Je, kwa nini Bunge lazima liridhie Mkataba wa Ushirikiano wa Kibiashara?

Bunge lina jukumu la kiserikali la kuridhia makubaliano yote ya kibiashara ili kuhakikisha kuwa yanajali masilahi ya nchi. Mkataba huu wa Ushirikiano wa Kibiashara, kama mikataba yoyote ya kibiashara, ulijadiliwa na Serikali Kuu na hivyo Bunge lazima liridhike kuwa utakuwa na faida kwa nchi na watu wa Kenya.

Katika Katiba ya Kenya ya 2010 na Sheria ya Uridhiaji wa Mikataba ya mwaka 2012, Bunge lina wajibu wa kutekeleza ushiriki wa umma kuhusu mkataba huu wa EPA na kuwasilisha ripoti ya maoni ya wadau. Hili lilifanyika. Bunge lilichapisha notisi ya ushiriki wa umma ikialika maoni ya wadau kuhusu EPA. Kamati ya Biashara, Viwanda na Ushirika iliandaa na kuwasilisha ripoti kwa Bunge.

Kwa nini Kenya na washirika wake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanahitaji Mkataba na Uingereza?

Uingereza ni moja ya washirika muhimu zaidi wa kibiashara na maendeleo kwa Kenya na nchi wanachama wa EAC. EPA itapanua fursa za kuimarisha ushirikiano huu.

EPA, ikiridhiwa na kutekelezwa, itakuwa na faida kubwa za kiuchumi na kijamii kwa nchi zinazofaidika. Itapanua na kuimarisha uhusiano wa kudumu na faida ya kiuchumi na kibiashara uliopo baina ya Uingereza na EAC. Aidha, itapanua fursa za bidhaa kutoka EAC kwenda EU na masoko mengine ya magharibi.

Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni kwa sekta muhimu za chumi za EAC unatarajiwa kuongezeka, haswa wakati Kenya na majirani zake wanapoendelea kuimarisha mageuzi ya mazingira ya uwekezaji ili kuhakikisha mazingira thabiti na bora ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Waliojadili mkataba walihakikisha kuwa makubaliano ya kibiashara yana usawa na yanalenga katika kuendeleza biashara yenye faida, uwekezaji na uhusiano wa kiuchumi baina ya Kenya na Uingereza.

Mchango wa Uingereza una umuhimu gani katika mchakato wa maendeleo ya Kenya?

Kenya na Uingereza zinafurahia ushirikiano wa muda mrefu, wenye faida katika biashara, uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni na maeneo mengine ya ushirikiano. Uingereza ni mwekezaji mkubwa zaidi wa kigeni nchini Kenya, kwa biashara inayokadiriwa kuwa pauni bilioni 2.7 (Shilingi bilioni 385).   Zaidi ya kampuni 220 za Uingereza zimewekeza katika sekta na maeneo yote nchini, na kuchangia ustawi wa kiuchumi na kijamii wa Kenya kupitia ajira, mapato na ukuaji wa uchumi.

Isitoshe, Uingereza ni mojawapo ya washirika wakuu wa kibiashara wa Kenya nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.   Thamani ya biashara ya kila mwaka kati ya nchi hizi mbili inakadiriwa kuwa Shilingi bilioni 70 hadi 90.

Kenya imendelea kuwa na usawa bora wa biashara tangu mwaka wa 2016. Faida ya juu zaidi kwa mwaka ilikuwa Shilingi bilioni 8.6 mwaka wa 2018, wakati thamani ya mauzo ya nje ya Kenya ilikuwa Shilingi bilioni 40.2, ikilinganishwa na uagizaji wenye thamani ya Shilingi bilioni 31.6. Kati ya Januari na Septemba 2020, Kenya ilipata Shilingi bilioni 37 kutoka kwa mauzo ya kwenda Uingereza na huku iliagiza bidhaa za Uingereza zenye thamani ya Shilingi bilioni 21.4, na kuletea Kenya faida ya biashara ya Shilingi bilioni 15.6.

Je, kutakuwa na athari gani ya makubaliano ya pande mbili kuhusu biashara kwa thamani na uanuai wa biashara kati ya nchi hizi mbili?

Kenya ni muuzaji wa nje mkubwa kwa Uingereza na Umoja wa Ulaya wa bidhaa za kilimo zikijumuisha chai, kahawa, maua, matunda na mboga.   Uingereza ndilo eneo la pili kwa ukubwa nje ya nchi, baada ya Uholanzi, kwa soko la maua yenye harufu nzuri kutoka Kenya, ikiwa na mgao wa soko ya asilimia 18. Kwa upande mwingine, Kenya inaagiza mashine za Uingereza, magari, mitambo ya nyuklia, boila, mitambo ya umeme na ya elektroniki, vinywaji na bidhaa za dawa. Makubaliano ya kibiashara yatalinda upendeleo wa soko kwa mauzo haya ya nje, huku yakiiwezesha Kenya kutafuta fursa za uanuai na kuimarisha uwepo wake katika masoko ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Je, wapatanishi walihakikisha kuwepo kwa usawa na usawazishi katika mazungumzo, hasa ikizingatiwa hadhi ya Uingereza kama mbabe wa kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani?

Kenya na Uingereza ziliongozwa na juhudi ya pamoja ya kujadili mfumo wa ushirikiano wa kibiashara na maendeleo unaofungamana na Sera ya Mambo ya Nje ya Uingereza kuhusu Afrika na Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Mauzo ya nje ya Kenya. Hiyo itasaidia kuchochea fursa za kuuza nje kwa mauzo ya nje yaliyopatiwa kipaumbele kwa ajili ya nyongeza ya thamani itakayosaidia ukuaji wa Biashara za Wastani na Ndogondogo (MSMEs). Kuboresha fursa hizi kutapanua mchango wa sekta ya MSME kwa ajira za vijana wa Kenya.

Kenya itaendelea kuboresha mazingira yake ya biashara, kupitia mageuzi ya hali ya uwekezaji, ili kutoa mazingira mazuri na thabiti kwa Uingereza na wawekezaji wengine wa kigeni. Katika Doing Business 2020 Benki ya Dunia inatambua Kenya kama kiongozi wa ulimwengu katika "kulinda haki za wawekezaji wachache" na wa nne bora katika "kupata mkopo". Kenya pia imerekodi ukuaji mkubwa katika maeneo mengine ya urahisi wa kufanya biashara.

Aidha, Kenya imetekeleza mfumo wa mageuzi utakaongeza Uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni, hususan katika sekta ya utengenezaji.  Kwa kutumia uwezo unaojitokeza kutoka kwa mfumo mpya wa ushirikiano unaothibitisha dhamira ya Serikali ya kutimiza Ajenda Nne Kuu na Ruwaza ya 2030. Itaimarisha zaidi nafasi ya Kenya kama kiingilio cha Afrika Mashariki na kukuza maendeleo katika nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki.

Je, Kenya itahakikishaje kuwa EPA haidhoofishi makubaliano yake na washirika wengine wa kibiashara?

Kenya na Uingereza zimeonyesha kujitoloea kwao kwa pamoja katika kulinda mpangilio wa kibiashara unaofungamana na kanuni za biashara za kimataifa za Shirika la Biashara Duniani. Makubaliano ya EPA pia yanafaa kuwezesha upekee na upendeleo wa Kenya katika biashara ya kidunia.

Aidha, washirika wote wamekubali kudumisha uaminifu wa makubaliano ya pande mbili ya biashara ya kimataifa ambayo Kenya imeweka na washirika wake wengine wa kibiashara, hususan katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA). Kenya na Uingereza zimewahakikishia mataifa wanachama wa EAC kuwa wako huru kujiunga na EPA, chini ya sheria na masharti yaliyokubaliwa baina ya Kenya na Uingereza.

Je, EPA inaendeleza ushindaji sawa kwa viwanda vyetu?

Makubaliano haya yanajumuisha vifungu mahsusi vya kulinda soko la Kenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kutoka ushindaji usio sawa wa wazalishaji kutoka Uingereza. EPA itawezesha uafikiaji wa bidhaa bila ushuru na vizuizi kutoka Kenya na mataifa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuingia soko la Uingereza. Kile ambacho Uingereza inatoa kwa Kenya na EAC ni msingi thabiti, wa kudumu na imara wa kuimarisha ufikiaji wao wa soko la Uingereza. Ufikiaji bure wa bidhaa za Uingereza kwa soko la Kenya na EAC utawekwa katika ushuru wa viwango na upunguzaji wa mgawo ambao utatekelezwa kwa zaidi ya miaka 25.

Je, bidhaa kutoka Uingereza kuja Kenya zitaacha kutozwa ushuru na kuwa na hadhi ya bure mara tu makubaliano yatakapoanza kutumika?

La. Kenya itaendelea kufanya asilimia 82.6 ya biashara baina yake na Uingereza kuwa huria polepole kwa kipindi cha miaka 25 lakini kuna kusitishwa kusitishwa kwa miaka saba. Hii inamaanisha kupunguzwa kwa ushuru kwa bidhaa za Uingereza zilizoingizwa Kenya na EAC kutaanza tu baada ya miaka saba na zitapungua kwa hatua zaidi kwa miaka 13. Uhuru wa bidhaa za Uingereza kuja Kenya ambao kwa sasa unatozwa ushuru wa asilimia 25 utaanza miaka 12 baada ya EPA kuanza kutumika na kupunguzwa zaidi polepole kwa miaka mingine 13. Hizi ni bidhaa zilizotengenezwa kamili ambazo  ni jumla ya asilimia 2.6 tu ya biashara ambayo Kenya na Uingereza wamekubaliana kufanya iwe huria, kwa hivyo, athari kwa uchumi kutokana na upunguzaji huo wa ushuru hautakuwa mkubwa sana.

 

Je, ni nini kitakachotokea kwa viwanda vinavyoweza kuwa vinazalisha bidhaa kama hizo nchini Kenya na washirika wengine wa EAC?

Makubaliano haya yana mifumo ya kulinda viwanda vichanga na uchumi wa Kenya na EAC. Usitishaji huo, pamoja na kupunguzwa kwa ushuru kwa hatua, unachukuliwa kuwa muhimu kulinda sekta ya utengenezaji nchini Kenya. Viwanda vyovyote vinavyotengeneza bidhaa kamili nchini Kenya na Washirika wengine wa EAC, vitakuwa na muda wa miaka 12 kujirekebisha kabla mfumo huria kuanza. Uwezo unaohitajika na hatua za ulinzi wa biashara zimekuwa zikitarajiwa katika Makubaliano ya Kibiashara baina ya Uingereza na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

 

Je, ni hatua na muda gani ulio muhimu katika utekelezaji wa EPA?

Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EPA) ulitiwa saini baina ya Kenya na Uingereza mnamo Desemba 2020 kufungua njia kwa uridhiaji kupitia michakato ya kitaifa na Mabunge nchini Kenya na Uingereza.

Mara tu utakaporidhiwa, Wizara ya Mambo ya Nje itaandaa na kuweka hati za uridhiaji huo kwenye hazina ya Serikali ya Uingereza. Mkataba huu utaanza kutumika pindi tu serikali hizi mbili zitakapobadilishana hati za uridhiaji ifikapo

Katikati ya mwezi wa Machi mnamo 2021na kuziweka kwenye hazina zinazohusika.

 

Wadau, wakiwemo walengwa, washirika, asasi za kiraia na vyombo vya habari, watahusika katika hatua zote muhimu za mchakato wa mazungumzo na utekelezaji.

Mchakato bora wa ushirikishwaji utaleta makubaliano ya kibiashara na ushirika  wa kiuchumi unaojumuisha wote na kukubalika utakaongoza mustakabali wa uhusiano kati ya Kenya na Uingereza, pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa hakika.

 

Februari 2021