Saba Saba: Maadhimisho Ya ‘Siku Ya Kiswahili Duniani’ Jijini Nairobi

NA PROF IRIBE MWANGI

SIKU ya Jumatatu nilipotembelea stesheni moja ya runinga nchini nilikutana na mshairi chipukizi kwa jina Mohamed Mwinyimsa anayeghani mashairi kwa namna inayonifanya kuona kuwa Nuhu Bakari ana wajukuu.

Iribe Mwangi, Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Nairobi

Mwinyimsa alijuzwa kwangu mkereketwa mkubwa wa Kiswahili, Wambugu Yusuf. Wote wawili waliniuliza swali, “Prof, kuna mipango ipi kuhusu maadhimisho ya siku ya Kiswahili?” Niliwajibu nilivyowezeshwa.

Siku iliyofuata Henry Indindi, mwanafunzi wangu wa zamani kama vile Yusuf, aliniuliza swali lilo hilo na jana, Jackton Nyonje, alitaka kujua kama kuna mipango yoyote ya kuadhmisha. Inadhihirika kwangu kwamba kuna wengi wanaojiuliza swali hili na kwa sababu hiyo naona bora kutoa maelezo machache nilioyonayo hapa, japo kwa kifupi.

Nijuavyo, maadhimisho yataanza leo saa nne asubuhi katika eneo la KICC.

Bendi ya askari wa wanyamapori itaongoza matembezi ya uhamasishaji kupitia Barabara ya Moi Avenue, Kipande Road hadi kwenye majengo ya National Museum.

Matembezi hayo yataanzishwa na Waziri wa Michezo, Turathi na Utamaduni Balozi Amina Mohammed akishirikiana na mwenzake wa Utalii na Wanyamapori Mhe. Najib Balala. Baadaye, mawaziri hawa wawili watashirikiana na wasomi wa Kiswahili na wageni wengine waalikwa katika kuitambua siku hii muhimu.

Katika eneo hilo la National Museum, kutakuwa na maonyesho anuai yanayohusu utamaduni wa WaSwahili kama vile vyakula na mavazi.

Kutakuwa na utumbuizaji wa nyimbo na mashairi. Wasomi na wapenzi wa Kiswahili pia watakuwa na kikao na watakadadavua mambo yanayohusu lugha ya Kiswahili na kuchunguza mustakabali wake wa sasa na wa baadaye.