TANZANIA YAANZISHA DARASA LA KWANZA LA KISWAHILI NCHINI MALAWI

Darasa la Kiswahili Nchini Malawi ni sehemu ya Jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ubalozi wake Nchini Malawi kukipeleka kiswahili nje kama Lugha, utamaduni na bidhaa. Darasa la kwanza limeendeshwa na Wataalam wa kiswahili kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na baadaye darasa hilo litaendelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Hebron cha Nchini Malawi.

 

Wiki hii ujumbe wa wataalam wa masuala ya Elimu kutoka Tanzania wakiongozwa na Prof. Nombo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia watakuwa na vikao na Taasisi za Serikali ya Malawi ikiwemo Wizara ya Elimu, Vyuo vya Ualimu na Vyuo Vikuu ili kuona namna bora ya kuimarisha mashirikiano ya kielimu na kwa umahususi kukileta kiswahili Malawi.